Saturday, February 9, 2013

TAARIFA YA WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA



TAARIFA
TAASISI YA WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
1.   UTANGULIZI
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Wanawake Mashujaa Tanzania ilianza shughuli zake rasmi mnamo mwaka 2011 tarehe   23.11 kikiwa kama chama kidogo kilichojitolea kusaidia jamii katika nyanja za familia na maendeleo kwa ujumla, hasa kwa kumlenga mwanamke zaidi. Kutokana na juhudi mbali mbali za ugaribishaji mwaka 2012, Wanawake Mashujaa Tanzania ilipata mafanikio makubwa na kukubalika miongoni mwa  jamii na hatimaye kuongeza wigo wa kusaidia jamii hasa baada ya wanaume kupenda huduma yetu na kuomba Wanawake Mashujaa Tanzania isiwe chama cha Wanawake tu, bali iwe Taasisi ambayo itakuwa ikisaidia wanawake na wanaume bila kusahau jamii inayotuzunguka

Kufikia mwaka 2012, Wanawake Mashujaa Tanzania ilifanikiwa kutoa huduma ya mafunzo ya saikolojia ya mahusiano, malezi ya watoto na jinsi ya kuishi na jamii kwa ujumla. Tulifanikiwa kufanya huduma za kijamii katika mji wa Arusha kama ifuatavyo;

·        Kuwatembelea watoto yatima siku za sikukuu
·        Kutembelea wagonjwa mahospitalini na kuwapa zawadi
·        Kuwatembelea wafungwa magerezani n.k

Tuliweza kutoa huduma ya ushauri na maadili mema kwa vijana wa rika la kati katika shule za msingi, sekondari na vyuo. Huko tulibaini mambo yafuatayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kumomonyoka kwa maadili katika jamii. Mambo hayo ni kama yafuatayo;

·        Kukosa  uvumilivu baina ya wazazi/walezi

·        Hakuna upendo wa dhati (wengi wanaishi maisha ya kuigiza)

·        Kukosa  uaminifu hadi mbele za watoto wetu

·        Wazazi/walezi wamesahau uwajibikaji katika malezi / kuwapa uhuru unaozidi.

·        Wazazi/walezi wamekosa utaratibu mzuri wa kupanga ratiba zao za kazi na kufanya kazi zaidi na kusahau kuangalia maendeleo ya watoto wao n.k


2.  MALENGO YA TAASISI 2013 - 2015
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Taasis ya Wanawake Mashujaa Tanzania ina malengo yafuatayo kwa mwaka 2013 - 2015 ni kama ifuatavyo;

·        Kufungua ofisi hapa Mkoani Singida itakayofanya kazi ikisaidiana na jamii katika kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii hasa katika saikolojia ya mahusiano na malezi ya watoto.

·        Kuanzisha mfuko wa taasisi ambao utasaidia katika huduma za kijamii hapa Singida kama kuwatembelea watoto yatima, wagonjwa na wafungwa alau mara moja kwa mwaka, kusaidiana wenyewe kwa wenyewe pale inapobidi.

·        Kuwa na darasa la kufundisha saikolojia ya mahusiano ikiwezekana mara moja kila mwezi.

·        Kuanzisha miradi mbali mbali itakayosaidia kuinua mitaji ya kina mama na mabinti walio katika mazingira magumu ambao hawana uwezo wa kuendelea na masomo tena.

·        Kuwa na miradi endelevu ili taasisi isiwe tegemezi kwa muda mrefu

·        Kufungua matawi ya taasisi Mikoa yote Tanzania na hatimae nje ya nchi.
3.  MAONO YA TAASISI
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Wanawake Mashujaa Tanzania ina maono yafuatayo katika kuhakikisha malengo yake yanafikika bila matatizo yoyote ifikapo mwaka 2015;

·        Tumejipanga kufanya kazi kwa juhudi zaidi, uaminifu wa hali ya juu, na kujitangaza zaidi katika jamii zote Tanzania na wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi.

·        Tupo tayari kushirikiana na mashirika mbali mbali kwa ajili ya kujifunza zaidi, na kufanya shughuli za jamii pamoja tukiamini ushirikiano ndio nguzo ya kutokomeza matatizo katika jamii.

·        Taasisi inakakaribisha wadau mbali mbali ili kufadhili huduma tunayoifanya kwa kusaidia katika uandaaji wa makongamano, wagarabishaji, na posho za wakufunzi ili kuweza kusaidia jamii husika na hatimae kujenga jamii iliyoimarika katika idara hizo mfano;  mabenki, wadau wa afya, wadau wa kilimo, wadau wa sheria, wadau wa biashara n.k


4.  CHANGAMOTO
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Taasisi ya Wanawake Mashujaa Tanzania imekuwa ikikutana na changamoto mbali mbali katika jamii kama ifuatavyo;

·        Tunashindwa kuzifikia jamiinyingine kutokana na ukosefu wa posho za wanaharakati, fedha za kujikimu tuwapo katika ziara vijijini na hata katika miji n.k

·        Ukosefu wa fedha za uendeshaji hasa pale tunapohitajika kusaidia jamii husika, wakitudhania kuwa tuna uwezo wa kuwasaidia kifedha.

·        Ukosefu wa ofisi maalumu ambayo itasaidia katika kukutana na wana jamii kwa uhuru na faragha zaidi pale wanapohitaji huduma ya ushauri.

·        Wakati mwingine tunakosa ushirikiano kutoka katika serikali ngazi ya kata na kijiji, hivyo inakuwa vigumu kuingia katika jamii na kuanza kujitambulisha kama wanaharakati wa mambo ya jamii, ili tuweze kujua ni matatizo gani wanakutana nayo ili tuweze kusaidiana nao katika kuyatatua.

5.  MWISHO
·        Tunapenda kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kutimiza mwaka mmoja, tukiwa wenye nguvu, maarifa, afya njema, na hekima zaidi za kutuwezesha kuanza mwaka mwingine kwa ari mpya na kasi mpya.

·        Kibinafsi napenda kumshukuru Mume wangu Patrick A. Mosha kwa kujali huduma ninayoifanya na kunisaidia kwa hali na mali ili kuhakikisha ndoto zangu za kuikomboa jamii ya Tanzania zinatimia.

·        Napenda kumshukuru mgeni rasmikwa kujali na kuja kutufungulia kongamano letu, ni faraja sana kuwa nawe siku ya leo, pia nawashukuru wageni wote mliotoka serikalini, wachungaji, waandishi wa habari, na wengine wote mliosafiri kutoka mbali kuja kuniunga mkono.

·        Nawashukuru washiriki wote mliokuja kunisapoti kwa kuchangia michango mbali mbali na hatimae kuhudhuria kongamano hili, naamini kwamba mpo katika Taasisi salama na Mungu atafanikisha yale yote mnayotamani kupata kutoka kwetu.

·        Tunawakaribisha wote kwa moyo mkunjufu, mjiskie mpo salama, wazungu wanasema ( WE ARE THE SHOULDER, YOU CAN LEAN ON US)

KARIBUNI SANA!

OMBI KWA MGENI RASMI
Ndugu Mgeni Rasmi, tunaomba mtutambue kama Taasisi inayosaidiana na serikali, pamoja na wadau mbali mbali katika kuikomboa jamii yetu hasa katika nyanja ya familia, ikimlenga Mwanamke ambaye ni nguzo ya Taifa, Mwanaume ni Simba wa Afrika na hatimaye mtoto ambaye ni Taa ya Afrika.

Ndugu Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vincent Kone, tumevutiwa na juhudi mbali mbali ambazo Mkoa wa Singida umekuwa ukizifanya chini ya uongozi wakothabiti. Aidha, tunatambua mafanikio mengi mazuri yaliyopatikana hapa Singida. Sasa hivi Singida inatambulika kama moja ya miji inayokuwa kwa kasi hapa nchini.

Katika ukusanyaji wangu wa taarifa mbali mbali hapa Singida nimepata taarifa kuwa Mkoa huu, hususani Mkoa wetu wa Singida upo katika jitihada za kupambana na tatizo sugu la watoto wa mitaani (STREET CHILDREN) Nitapenda Taasisi hii kuwa sehemu muhimu ya juhudi hizo. Vile vile natambua kuwa manispaa ya Singida ina mkakati mahususi wa kuondokana na tatizo hilio, kinachopungua ni juhudi za wadau mbali mbali wa maendeleo. Tupo tayari kwa kukabiliana na changamoto hii.

Ombi letu ni kupata ufadhili wa fedha ili tuweze kununua eneo na  kujenga kituo cha watoto yatima waliojaa mitaani na kuwasaidia wale wenye mazingira magumu pale inapobidi ili warudi katika familia zao au wapate shughuli za kufanya na wanaopaswa kurudi shule tusaidiane warudi shule.

·        Ndugu Mgeni Rasmi, tunaimani ya kuwa ombi letu litafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo ili mwaka huu tuanze shughuli hiyo rasmi ya kulea watoto yatima.




Imeandaliwa na kusomwa na Mwanamke Shujaa Tanzania

………………………………
BI. DIANA DIDAS SHIRIMA (MRS. DIANA PATRICK MOSHA)
MUANZILISHI – WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
+255 766 44 57 33/ 682 622 626/ 765 99 71 99

No comments:

Post a Comment