Monday, June 4, 2012

Darasa la Mapenzi: KUPATA MAPENZI UYATAKAYO KATIKA NDOA

Darasa la  Mapenzi:

KILA ndoa ina matatizo, na yanaweza kufumuka wakati wowote. La muhimu ni kwamba unapokuwa umeamua kujiingiza katika maisha ya ndoa unapaswa kujifunza jinsi ya kukabiliana na matatizo hayo ili yaweze kuisha salama na ndoa kuendelea kuwa salama.

Bila kujali umeenda umbali gani katika barabara hii ya ndoa, zipo kanuni rahisi lakini za muhimu za usalama katika barabara hii. Si rahisi sana kuzitekeleza kanuni hizi, kwa wanandoa walio wengi, lakini ni lazima kuzitekeleza iwapo wahusika wanapenda ndoa yao iwe salama.

Iwapo utazingatia kanuni hizi, utaifanya ndoa yako kuwa imara zaidi. Katika usalama huu utapata pia marupurupu – furaha, ngono, kuaminiana (kuaminiwa), mapenzi moto moto na kadhalika. Hebu sasa na tuziangalie kanuni zenyewe: -

1. ONESHA MATENDO YA KIMAHABA
Usipojishughulisha kwa lolote lile kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako utasababisha mwenzako achoke na hata kufikia mahala akakasirika. Ili kuepuka haya, hakikisha kuwa unayapa kipaumbele mambo ambayo yanamfanya mpenzi wako kujihisi maalumu kwako. Na njia rahisi zaidi ni kuwekeza katika matendo madogo madogo ya kimahaba.

Kumbuka, kauli moja hasi au ya kuvunja moyo inaweza kuhitaji kauli kama ishirini chanya ili iweze kufifia (si kufutika) akilini mwa mpenzi wako. Hii ina maana kwamba, badala ya kumlaumu mpenzi wako, wekeza zaidi katika kumsifia katika mambo yake, au mambo anayoyafanya utakavyo.

Msifie mpenzi wako kwa nguo yake mpya, msifie kwa kukujali, mpigie simu ofisini kwake na kumwambia kuwa ulikuwa unamuwaza na kadhalika. Isipokuwa, hakikisha kuwa sifa hizi na kauli hizi za mahaba zinadhihirika kutoka moyoni, zisije kuwa kama mazoea tu.

Iwapo utafanya hivi, ni rahisi sana kumfurahisha mpenzi au mwenzi mwenye nia njema na wewe. Kumbuka mambo yenu yalianza hivi hivi, pale mlipokuwa bado mnafukuziana. Matendo madogo ya kimahaba hayapaswi kuwa na mwisho, maana ndiyo hudumisha msisimko wa wenza.

2. TUMIA HISIA ZA MGUSO
Hisia za mguso ni muhimu sana kwa wapenzi. Na njia mojawapo ya kumweka mpenzi wako katika utayari wa kukupa kila kitu ni kumshika mkono unapotembea naye kwenda dukani. Naam, Afrika hii unaweza kusemwa na hata kuchekwa, lakini la muhimu kwako ni kwamba unamfanyia mwenzi wako wa maisha.

Unapomsalimia mwenzi wako, gusa mashavu yake kwa ncha za vidole vyako. Jikumbushe jinsi ulivyokuwa unamgusa katika siku za kwanza, kabla hujamzoea. Ulikuwa ukimgusa kwa huba na tamaa kubwa. Mbusu kila panapoweza kubusika, pitisha mkono wako kwenye nywele zake, na kadhalika. Kugusa ni lugha muhimu ya mapenzi. Itaongeza msamiati wako wa mapenzi.

Sanjari na kumgusa, onesha pia kuwa unamuunga mkono mwenzako. Unapotokea ugomvi, wewe nenda upande wa mwenzi wako. Pia mtunzie siri zake maana wewe ndiwe mwandani wake. Hata kama huko kazini au kokote watu watazungumza siri za wenzi wao, wewe siri za mwenzako ziache kuwa baina yake na wewe.

3. KUMBUKA HAKUNA MKAMILIFU
Unapokasirika, au kukatishwa tamaa, au kuvunjwa moyo au kufadhaishwa, unaweza kushindwa kujizuia kumlaumu aliyekusababishia hali hiyo, hata kama mtu mwenyewe ni mwenzi wako wa maisha. Pia, ni kawaida kwa mtu kujaribu kumbadilisha mpenzi wake anapodhani ana udhaifu fulani.

Hata hivyo, unapojaribu kumkosoa na kumrekebisha mpenzi au mwenzi wako unamweka katika hali ya kujitetea. Matokeo yake ni kwamba hatabadilika na pengine ataacha kuwajibika. Matokeo mengine ni kwamba furaha yake itaondoka. Kumbuka, unapomkosa mwenzako ni kama vile unapuuza asilimia 90 ya hulka yake njema ambayo ilikufanya uvutiwe kuwa naye.

Kama kweli unataka kumpa kipaumbele mwenzako na kisha kutarajia mazuri kutoka kwake, basi badala ya kutaka kumbadilisha yeye, badilika wewe mwenyewe kwa kuondoa mapungufu yako mwenyewe. Iwapo utajirekebisha, mpenzi wako hatasubiri umlaumu au umgombeze, bali yeye pia atabadilika.

Katika suala hili, ni vema kutambua kuwa hakuna mtu mkamilifu – si wewe, wala yeye, wala mwingine. Mungu tu ndiye mkamilifu. Siku nyingine mpenzi wako akifanya jambo ambalo unahisi linakukera, acha kuhemka. Badala yake, jifariji kwamba alikuwa na lengo zuri japo matokeo hayakuwa mazuri. Na kila siku, wiki au mwezi, chagua jambo moja ambalo unaliona kuwa zuri kwake, kisha litaje. Linaweza kuwa ucheshi, utani na kadhalika. Yaangalie hayo yaliyo chanya tu.

4. FAHAMU KUGOMBANA VIZURI
Migogoro katika ndoa ni kitu cha kawaida. Naam, wengine husema ndoa isiyo na migogoro ni sawa na kusema imekufa. La muhimu ni vile unavyokabiliana na migogoro hiyo.

Kwa hakika, kushirikiana katika kutatua migogoro ni vema zaidi kuliko kuhangaika mwenyewe. Naam, kama kila mmoja atakuwa na nia njema, migogoro inaweza kuwa njia mojawapo ya kuzidi kushikamana na mwenzako. Ni kwa kufahamu namna njema ya kukabiliana na migogoro ndipo mtu huweza kumpenda mwenzake kama alivyo.

Kumlaumu mwenzako ni kitu cha kuepuka kwa gharama yoyote. Pia, acha kukabiliana naye kwa maneno, kwani utakuwa unawasha moto ambao haitakuwa rahisi sana kuuzima. Wanandoa wenye furaha ni wale ambao huepuka sana kutumia vinywa vyao dhidi ya wenzao. Hawa hufahamu jinsi ya kuzuia mazungumzo kulipuka na kuwa ugomvi. Watu hawa hujitahidi kuepuka maneno ya kujiapiza kama “kamwe” na kadhalika.

Iwapo ugomvi utatokea (naam, hakika utatokea), jaribu kubadilisha mada, ingiza ucheshi, mwoneshe mwenzako mapenzi ya ziada. Kama utabaini kuwa tayari umechelewa, tafuta suluhu kwa kuondoka kwanza na kurudi baadaye kuendelea kuzungumza kila mmoja anapokuwa katika nafasi nzuri ya kutumia vema akili yake.

5. ZUNGUMZA NAYE KWA MUDA MUAFAKA
Usianzishe mazungumzo magumu au makali na mwenzi wako kama hauko mahala muafaka na wakati pia si muafaka. Njaa na uchovu vinaweza kusababisha mtu kujibu hovyo au kutojali. Pia si vema kumuuliza jambo mwenzako iwapo mmoja au nyote mmepata kileo.

Vilevile, epuka kuzungumzia masuala magumu ya kimahusiano iwapo jicho la pili litakuwa limeelekezwa kwenye kitu kingine. Zima TV, pia zima simu na laptop. Kama ulikuwa unasoma gazeti, lifunike ndipo uanze kuzungumza na mwenzako masuala nyeti ya kimaisha. Kama ukiona mazingira hayaruhusu, chagua wakati mwingine.

Lakini pia, kabla hujaanza mazungumzo na mwenzako, jiulize iwapo hutasababisha rabsha. Jiulize, je, mazungumzo yetu yataisha kwa furaha? Kama utabaini kuwa yanaweza yasiishe kwa furaha basi acha na kupanga siku nyingine.

6. TUMIA VEMA MASIKIO YAKO
Jambo hili la mwisho ni muhimu sana katika kuimarisha uhusiano wa kindoa. Ukitaka kupunguza migogoro baina yako na mwenzako, jifunze kuzungumza kidogo na badala yake kuwa msikivu zaidi. Kauli za lawama, matusi, kukosoa na nyingine za aina hiyo hubashiri mwisho wa uhusiano. Na hata kama uhusiano hautaisha lakini ni rahisi ndoa kuwa ndoana.

Mazungumzo yako na mwenzako yanapoanza kuchemka na kuonekana kama vile yanaelekea kubaya, epuka kumkata kauli mwenzako – iwe ni kwa kutoa suluhisho au kujitetea. Mwenzako anapokuwa na kitu kifuani, anataka kusikilizwa. Kwa hiyo msikilize na uoneshe kuwa unamsikiliza kwa kutikisa kichwa (juu-chini), au kumwitikia kwa mguno wa kumwonesha kuwa unamsikiliza na kuheshimu maneno yake.

TIMIZA WAJIBU WAKO
Iwapo utayazingatia mambo haya sita utakuwa umejenga msingi imara kwa mpenzi wako kuwa wazi kwako na kukupa mapenzi yote. Namna hii, japo ndoa yenu inaweza kupita kwenye misukosuko mara kwa mara, lakini itaibuka kidedea.

No comments:

Post a Comment