Saturday, February 9, 2013

TAARIFA YA WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA



TAARIFA
TAASISI YA WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
1.   UTANGULIZI
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Wanawake Mashujaa Tanzania ilianza shughuli zake rasmi mnamo mwaka 2011 tarehe   23.11 kikiwa kama chama kidogo kilichojitolea kusaidia jamii katika nyanja za familia na maendeleo kwa ujumla, hasa kwa kumlenga mwanamke zaidi. Kutokana na juhudi mbali mbali za ugaribishaji mwaka 2012, Wanawake Mashujaa Tanzania ilipata mafanikio makubwa na kukubalika miongoni mwa  jamii na hatimaye kuongeza wigo wa kusaidia jamii hasa baada ya wanaume kupenda huduma yetu na kuomba Wanawake Mashujaa Tanzania isiwe chama cha Wanawake tu, bali iwe Taasisi ambayo itakuwa ikisaidia wanawake na wanaume bila kusahau jamii inayotuzunguka

Kufikia mwaka 2012, Wanawake Mashujaa Tanzania ilifanikiwa kutoa huduma ya mafunzo ya saikolojia ya mahusiano, malezi ya watoto na jinsi ya kuishi na jamii kwa ujumla. Tulifanikiwa kufanya huduma za kijamii katika mji wa Arusha kama ifuatavyo;

·        Kuwatembelea watoto yatima siku za sikukuu
·        Kutembelea wagonjwa mahospitalini na kuwapa zawadi
·        Kuwatembelea wafungwa magerezani n.k

Tuliweza kutoa huduma ya ushauri na maadili mema kwa vijana wa rika la kati katika shule za msingi, sekondari na vyuo. Huko tulibaini mambo yafuatayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kumomonyoka kwa maadili katika jamii. Mambo hayo ni kama yafuatayo;

·        Kukosa  uvumilivu baina ya wazazi/walezi

·        Hakuna upendo wa dhati (wengi wanaishi maisha ya kuigiza)

·        Kukosa  uaminifu hadi mbele za watoto wetu

·        Wazazi/walezi wamesahau uwajibikaji katika malezi / kuwapa uhuru unaozidi.

·        Wazazi/walezi wamekosa utaratibu mzuri wa kupanga ratiba zao za kazi na kufanya kazi zaidi na kusahau kuangalia maendeleo ya watoto wao n.k


2.  MALENGO YA TAASISI 2013 - 2015
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Taasis ya Wanawake Mashujaa Tanzania ina malengo yafuatayo kwa mwaka 2013 - 2015 ni kama ifuatavyo;

·        Kufungua ofisi hapa Mkoani Singida itakayofanya kazi ikisaidiana na jamii katika kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii hasa katika saikolojia ya mahusiano na malezi ya watoto.

·        Kuanzisha mfuko wa taasisi ambao utasaidia katika huduma za kijamii hapa Singida kama kuwatembelea watoto yatima, wagonjwa na wafungwa alau mara moja kwa mwaka, kusaidiana wenyewe kwa wenyewe pale inapobidi.

·        Kuwa na darasa la kufundisha saikolojia ya mahusiano ikiwezekana mara moja kila mwezi.

·        Kuanzisha miradi mbali mbali itakayosaidia kuinua mitaji ya kina mama na mabinti walio katika mazingira magumu ambao hawana uwezo wa kuendelea na masomo tena.

·        Kuwa na miradi endelevu ili taasisi isiwe tegemezi kwa muda mrefu

·        Kufungua matawi ya taasisi Mikoa yote Tanzania na hatimae nje ya nchi.
3.  MAONO YA TAASISI
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Wanawake Mashujaa Tanzania ina maono yafuatayo katika kuhakikisha malengo yake yanafikika bila matatizo yoyote ifikapo mwaka 2015;

·        Tumejipanga kufanya kazi kwa juhudi zaidi, uaminifu wa hali ya juu, na kujitangaza zaidi katika jamii zote Tanzania na wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi.

·        Tupo tayari kushirikiana na mashirika mbali mbali kwa ajili ya kujifunza zaidi, na kufanya shughuli za jamii pamoja tukiamini ushirikiano ndio nguzo ya kutokomeza matatizo katika jamii.

·        Taasisi inakakaribisha wadau mbali mbali ili kufadhili huduma tunayoifanya kwa kusaidia katika uandaaji wa makongamano, wagarabishaji, na posho za wakufunzi ili kuweza kusaidia jamii husika na hatimae kujenga jamii iliyoimarika katika idara hizo mfano;  mabenki, wadau wa afya, wadau wa kilimo, wadau wa sheria, wadau wa biashara n.k


4.  CHANGAMOTO
Ndugu, Mgeni Rasmi,
Taasisi ya Wanawake Mashujaa Tanzania imekuwa ikikutana na changamoto mbali mbali katika jamii kama ifuatavyo;

·        Tunashindwa kuzifikia jamiinyingine kutokana na ukosefu wa posho za wanaharakati, fedha za kujikimu tuwapo katika ziara vijijini na hata katika miji n.k

·        Ukosefu wa fedha za uendeshaji hasa pale tunapohitajika kusaidia jamii husika, wakitudhania kuwa tuna uwezo wa kuwasaidia kifedha.

·        Ukosefu wa ofisi maalumu ambayo itasaidia katika kukutana na wana jamii kwa uhuru na faragha zaidi pale wanapohitaji huduma ya ushauri.

·        Wakati mwingine tunakosa ushirikiano kutoka katika serikali ngazi ya kata na kijiji, hivyo inakuwa vigumu kuingia katika jamii na kuanza kujitambulisha kama wanaharakati wa mambo ya jamii, ili tuweze kujua ni matatizo gani wanakutana nayo ili tuweze kusaidiana nao katika kuyatatua.

5.  MWISHO
·        Tunapenda kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kutimiza mwaka mmoja, tukiwa wenye nguvu, maarifa, afya njema, na hekima zaidi za kutuwezesha kuanza mwaka mwingine kwa ari mpya na kasi mpya.

·        Kibinafsi napenda kumshukuru Mume wangu Patrick A. Mosha kwa kujali huduma ninayoifanya na kunisaidia kwa hali na mali ili kuhakikisha ndoto zangu za kuikomboa jamii ya Tanzania zinatimia.

·        Napenda kumshukuru mgeni rasmikwa kujali na kuja kutufungulia kongamano letu, ni faraja sana kuwa nawe siku ya leo, pia nawashukuru wageni wote mliotoka serikalini, wachungaji, waandishi wa habari, na wengine wote mliosafiri kutoka mbali kuja kuniunga mkono.

·        Nawashukuru washiriki wote mliokuja kunisapoti kwa kuchangia michango mbali mbali na hatimae kuhudhuria kongamano hili, naamini kwamba mpo katika Taasisi salama na Mungu atafanikisha yale yote mnayotamani kupata kutoka kwetu.

·        Tunawakaribisha wote kwa moyo mkunjufu, mjiskie mpo salama, wazungu wanasema ( WE ARE THE SHOULDER, YOU CAN LEAN ON US)

KARIBUNI SANA!

OMBI KWA MGENI RASMI
Ndugu Mgeni Rasmi, tunaomba mtutambue kama Taasisi inayosaidiana na serikali, pamoja na wadau mbali mbali katika kuikomboa jamii yetu hasa katika nyanja ya familia, ikimlenga Mwanamke ambaye ni nguzo ya Taifa, Mwanaume ni Simba wa Afrika na hatimaye mtoto ambaye ni Taa ya Afrika.

Ndugu Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vincent Kone, tumevutiwa na juhudi mbali mbali ambazo Mkoa wa Singida umekuwa ukizifanya chini ya uongozi wakothabiti. Aidha, tunatambua mafanikio mengi mazuri yaliyopatikana hapa Singida. Sasa hivi Singida inatambulika kama moja ya miji inayokuwa kwa kasi hapa nchini.

Katika ukusanyaji wangu wa taarifa mbali mbali hapa Singida nimepata taarifa kuwa Mkoa huu, hususani Mkoa wetu wa Singida upo katika jitihada za kupambana na tatizo sugu la watoto wa mitaani (STREET CHILDREN) Nitapenda Taasisi hii kuwa sehemu muhimu ya juhudi hizo. Vile vile natambua kuwa manispaa ya Singida ina mkakati mahususi wa kuondokana na tatizo hilio, kinachopungua ni juhudi za wadau mbali mbali wa maendeleo. Tupo tayari kwa kukabiliana na changamoto hii.

Ombi letu ni kupata ufadhili wa fedha ili tuweze kununua eneo na  kujenga kituo cha watoto yatima waliojaa mitaani na kuwasaidia wale wenye mazingira magumu pale inapobidi ili warudi katika familia zao au wapate shughuli za kufanya na wanaopaswa kurudi shule tusaidiane warudi shule.

·        Ndugu Mgeni Rasmi, tunaimani ya kuwa ombi letu litafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo ili mwaka huu tuanze shughuli hiyo rasmi ya kulea watoto yatima.




Imeandaliwa na kusomwa na Mwanamke Shujaa Tanzania

………………………………
BI. DIANA DIDAS SHIRIMA (MRS. DIANA PATRICK MOSHA)
MUANZILISHI – WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
+255 766 44 57 33/ 682 622 626/ 765 99 71 99

Hatimaye Wanawake Mashujaa Tanzania imezinduliwa rasmi leo mkoani Singida!

Wapendwa Wanaharakati wa wanawake mashujaa Tanzania, napenda kuwahabarisha kuwa Taasisi yetu imesajiliwa leo rasmi kama Taasisi inayosaidiana na Jamii na Serikali ili kuweza kutengeneza jamii imara katika nyanja ya familia na malezi ya watoto.

Tunamshukuru Mh. Manju Salum Msambya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi kwa kujali na kuja kufungua kongamano letu la ufunguzi wa Kongamano la Wachumba na Wanandoa ili kuweza kufanya shughuli zake rasmi hapa Singida na nje ya Singida.

Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida Dct. Parseko Vincent Korne, kwa kujali mualiko wetu na kuweza kutupa Mgeni Rsmi anaye muamini na kumtambua kazi yake vizuri ili kuwa mgeni raasmi, Napenda kutoa shukurani kwa serikali, Mshauri mkuu wa Taasisi ya Wanawake Mashujaa Tanzania ndugu, Selestine Onditi (DAS) SINGIDA. Kwa mchango wake mkubwa alioonesha hadi kufanikisha ufunguzi huu.

Nawashukuru wadau wote na washiriki wote waliojali na kuchangia kwa hali na mali katika kushiriki kongamano la wapendanao, tuna amini huu ni mwanzo mzuri na ushindi ni mkubwa.

Sitaacha kumshukuru MC wangu maarufu na mashuhuri kutoka Arusha, Mc Rosse Mosha aka PRETTY LADY Mungu ambariki sana na endapo utakuwa unahitaji shughuli yoyote ya kitchen party, sendoff, harusi n.k usisite kumtafuta! +255 767233323/255789647694

Friday, January 18, 2013

INAPENDEZA SANA KULA CHAKULA PAMOJA NA FAMILIA YAKO

Nawasalimu sana wapendwa wangu, leo napenda kuzungumzia jinsi mfumo wa kula pamoja na familia yako unavyoweza kukusaidia katika kuijuwa familia yako vizuri, tukianza na mama, baba na watoto pia ni vyema kama kuna kijana/ binti wa kazi awepo pia katika meza ya chakula.

Faida ambazo mtazipata zitafanana na hizi endapo mtasimama katika jambo hili ipasavyo.
  • Kufahamu usalama wa wale unaowahudumia hapo ndani, nikimaanisha kuwa mkila pamoja mezani mtaweza kuhakiki nani yupo mezani na nani hayupo mezani  na ni kwa nini?
  • Pili mtaweza kufahamu ambaye hayupo ana tatizo gani, au ni mgonjwa au ni mjamzito n.k
  • Tatu mtakapo maliza kula mnaweza kujadili mambo mbali mbali yahusuyo familia yako ukiwa kama baba na mama, mtaweza kusikiliza maoni ya watoto wenu kuhusu mwenendo mzima wa familia na wanavyoishi shuleni na katika jamii iliyowazunguka.  
HASARA
  • Hasara zinazoweza kutokea ni kutojuwa familia yako kwa undani, hii inatokana na kutokuwa na ratiba nzuri juu ya familia yako.
  • Watoto wako na jamii yako vitaweza kupotea kutokana na kutokuwa na ulinzi mzuri kiasi cha kwamba mwisho wa siku unajutia uzazi wako.
  • Mabinti zetu wanabeba mimba na hata wazazi/walezi hawajui chochote hadi anakuja kukuta mtoto anakaribia kujifungua ndo mzazi anashtuka.
  • Kutofahamu hali ya maisha wanayoishi wanafamilia yako, n.k

WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA: NDUGU MZAZI/MLEZI UNAFAHAMU KIJANA WAKO ANA MARAFI...

WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA: NDUGU MZAZI/MLEZI UNAFAHAMU KIJANA WAKO ANA MARAFI...: Vijana wengi walio na malezi mazuri huwa waoga sana kujiingiza katika makundi ya watoto wenye malezi mabaya, hii ni kutokana na ...

NDUGU MZAZI/MLEZI UNAFAHAMU KIJANA WAKO ANA MARAFIKI WA AINA GANI?





Vijana wengi walio na malezi mazuri huwa waoga sana kujiingiza katika makundi ya watoto wenye malezi mabaya, hii ni kutokana na uangalizi wa wazazi/walezi.

Tunafanyaje katika jambo hili? Wengi wetu tumekuwa bize sana na kazi na biashara kuliko kusimamia swala zima la malezi. Watoto wetu wamekuwa wakivutwa na makundi mabaya sana kutokana na upweke walionao nyumbani, kwani wanakosa watu wa kuwasaidia kimawazo na kuwafundisha watoto wao jinsi ya kujisaidia kimawazo.

Tusifanye kazi sana hadi kusahau watoto wetu, hawa ndio wanaotufanya sisi tushindwe kukaa nyumbani na kuahangaikia, sasa endapo tutawasahau itakuwa haina maana kabisa kwani mwisho wa siku hakuna maana yoyote ya kuhangaika.

Suluhu ni nini?

Hakikisha una ratiba ya kudumu kwa ajili ya watoto na familia kwa ujumla ili kutengeneza mambo mazuri kwa familia yako, ukipanga ratiba zako utaweza kujua binti / kijana wako anachojifunza katika marafiki zake na endapo utaona marafiki zake ni wale wenye maadili mabaya basi utaweza kumsaidia kabla hajaharibika zaidi.

Monday, December 17, 2012

KONGAMANO, KONGAMANO, KONGAMANO, BADO TUNAJIANDAA KWA KUNGAMANO KABAMBE HAPA SINGIDA!



KARIBU KATIKA KONGAMANO LA WANANDOA/WALIO KATIKA SAFARI YA KUINGIA KATIKA NDOA 2013 HAPA NYUMBANI SINGIDA

MAHALI: SOCIAL HALL — RC SINGIDA
SAA:  5:00 - 10:30 JIONI ( kutakuwa na chakula cha mchana pamoja na kinywaji)

COUPLES 100 ZA KWANZA ZITAPEWA ZAWADI MAALUMU KWA AJILI YA VALENTINE DAY!

TAREHE YA MWISHO KUJIANDIKISHA: 25.01.2013 USIKOSE

Wanawake Mashujaa Tanzania inapenda kukupa habari njema wewe mume/mke au nyie wachumba mnaotegemea kuingia kwenye ndoa na yeyote yule ambaye anafikiria siku moja kuingia katika ndoa kutakuwa na siku yenu tarehe 9/2/2013. Wasemaji maarufu kutoka sehemu mbalimbali Tanzania watakuwepo, hii ni kwa mara ya kwanza kutokea mkoani  Singida sio  ya kukosa mtaarifu jirani yako, shoga yako, shemeji, wifi wote mnakaribishwa.

Kiingilo Wawili(double) 40,000/= na 
mmoja(single)  20,000/=  chakula na viburudisho

Usisahau rangi ya siku ni NYEKUNDU NA NYEUPE.
 (Kwa wadada  kitenge kitapendeza zaidi)
Zawadi zitatolewa mlangoni kwa couples (wapendanao) zitakazokuwa zimependeza zaidi. Pia kutakuwepo na zulia jekundu kwa ajili ya kuchukulia picha kwa wale watakaopendeza zaidi.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na
Diana D. Shirima
Mwanzilishi - Wanawake Mashujaa Tanzania
Simu namba. . +255 766 44 57 33 / 682 622 626
www.wanawakemashujaatanzania.blogspot.com

Mr. Patrick Mosha  +255 787 99 71 99
patmo81@yahoo.com



UKIPIGA SIMU NITAKUELEKEZA TIKETI ZINAPATIKANA WAPI KATIKA ENEO ULILOPO!

Monday, December 3, 2012

MUONGOZO WA KANUNI ZINAZOMTAMBULISHA MWANAMKE SHUJAA TANZANIA



WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA

MWONGOZO WA KILA MWANACHAMA
         
1.  UHALISI WA MAISHA:
Kila mwanachama wa chama cha  WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
anatarajiwa kuishi maisha halisi ya mwanamke anayetarajia kuwa
mke/ mke tayari hii ni kumaanisha kuwa wanawake mashujaa tunapaswa kuishi maisha ambayo yanatutambulisha kama mfano wa kuigwa ili tunapozungumza na kufundisha mabadiliko tuwe tunazungumza uhalisia wa maisha yetu ambao unajengwa na haya yafuatayo;

2.  UVUMILIVU:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa mvumilivu katika maisha yake ya kila siku hasa ukizingatia kuwa tunakutana na mambo mbali mbali yasiyotuvutia katika mahusiano yetu, mengine ni magumu na yanayokwenda kinyume kabisa na matakwa yetu au mazoea yetu ya binafsi. Ifahamike kwamba wewe kama mwanamke shujaa inapotokea umekutana na mambo kama haya hupaswi kuonyesha hasira zako wazi wazi kama vile; chuki, kulaumu, ugomvi, vurugu, malalamiko, manung’uniko, machafuko, kulipa kisasi au aina yoyote ya uharibifu kutokea kwako au ndani mwako. Hivyo mwanamke shujaa huwa ni heri kila anapokuwa kwani hutunza amani ya eneo alipo.

3.  UPENDO WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa akiishi maisha ya upendo wa halisi na sio wa kinafki kwa jamii inayomzunguka. Tabia ya upendo wa halisi ina thamani kubwa sana kuliko mali nyingi, pesa, elimu ya juu n.k. wewe unaweza kabisa kuwa na elimu ya juu sana na pesa nyingi sana lakini pasipo upendo wa halisi ni sawa na kusema kopo zuri kwa nje na ndani hamna kitu. Nguzo kuu ya maisha ya mwanamke shujaa ni Upendo wa dhati na uhalisia.

4. UTII KWA KWA JAMII:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya utii katika jamii inayokuzunguka  ili kuweza kuyafanyia kazi yale yote uliyojifunza na pia kuyatenda kwa ufasaha pasipo kupita kona yoyote. Utii  kwa jamii ni ufunguo mmoja wapo utakaokusaidia kufanikisha mambo yako na malengo yako kama mwanamke shujaa.

5.  UAMINIFU KATIKA JAMII:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha ya uaminifu wa kweli na uhalisia katika jamii inayomzunguka. Uaminifu wa kweli huonekana nyakati zote na siyo tu wakati mtu anapokuwa mbele za watu wanaomjua bali hata wale wasiomjua na hata anapokuwa mahali peke yake aweze kutunza uaminifu wake kwa faida ya jamii nzima. Mwanamke shujaa hujitahidi sana kutunza uaminifu wake katika sekta zote.

6.  UNYENYEKEVU WA KWELI:
Kila mwanachama anatarijiwa kuishi maisha halisi kabisa ya unyenyekevu kwa jamii inayomzunguka, unyenyekevu ni kinyume
kabisa na kiburi, majivuno, kujigamba, kujikweza, kujiinua, kujiona,
na hata kjitanguliza mbele kwa kila jambo. Mwanamke shujaa huwa ni mnyenyekevu wakati wote na hana makuu daima.

7.  UWAJIBIKAJI WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya uwajibikaji akiangalia majukumu yake yote yanayomkabili na kuhakikisha anafanya kwa moyo bila kuwa na tabia ya kusaidiwa majukumu yake. Mwanamke shujaa ni mfano wa kuigwa kutokana na uwajibikaji wake.

8.  USHIRIKIANO WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya ushirikiano katika jamii inayomzunguka. Sisi wanawake mashujaa yatupasa kujua dhahiri kuwa kazi ya kubadili tabia na kufanya wengine wabadilike kwa lengo la kupata familia bora ni lazima kuwa na ushirikiano wa kweli ambao utajenga tabia ya kuaminiana na kunai mamoja katika harakati hizi za kuandaa/ kujenga familia bora.

9.   UTARATIBU WA KAZI/MPANGILIO:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa na maisha ya uhalisia katika utaratibu wa maisha yake, pamoja na mpangilio mzuri wa mambo yanayomzunguka hii itakusaidia kuwa na muda mzuri wa kufanya shughuli zako na pia kutekeleza majukumu yako ya kila siku kama mwanamke shujaa. Hakuna njia yoyote ya kukuwezesha kukua na kuendelea katika maisha yako bila kuwa na utaratibu na mpangilio wa mambo yako.
10.  KUFANYA TATHIMINI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha ya halisi ya kuweza kufanya tathimini ya yale yote anayoyafanya katika maisha yake ya kila siku, pengine ni mfanyabiashara, mfanyakazi, mkulima n.k kama mwanamke shujaa yakupasa kutathimini shughuli zako kama zina leta faida/hasara kwa familia na jamii yako inayokuzunguka. Ukiona faida ni kubwa unaendelea na hiyo shughuli lakini kama hasara ni kubwa unajiweka katika nafasi ya kubadilisha aina ya shughuli mara moja bila kupoteza wakati.





Imeandaliwa na:
Diana Didas Shirima
Founder - Wanawake Mashujaa Tanzania