Monday, December 3, 2012

MUONGOZO WA KANUNI ZINAZOMTAMBULISHA MWANAMKE SHUJAA TANZANIA



WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA

MWONGOZO WA KILA MWANACHAMA
         
1.  UHALISI WA MAISHA:
Kila mwanachama wa chama cha  WANAWAKE MASHUJAA TANZANIA
anatarajiwa kuishi maisha halisi ya mwanamke anayetarajia kuwa
mke/ mke tayari hii ni kumaanisha kuwa wanawake mashujaa tunapaswa kuishi maisha ambayo yanatutambulisha kama mfano wa kuigwa ili tunapozungumza na kufundisha mabadiliko tuwe tunazungumza uhalisia wa maisha yetu ambao unajengwa na haya yafuatayo;

2.  UVUMILIVU:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa mvumilivu katika maisha yake ya kila siku hasa ukizingatia kuwa tunakutana na mambo mbali mbali yasiyotuvutia katika mahusiano yetu, mengine ni magumu na yanayokwenda kinyume kabisa na matakwa yetu au mazoea yetu ya binafsi. Ifahamike kwamba wewe kama mwanamke shujaa inapotokea umekutana na mambo kama haya hupaswi kuonyesha hasira zako wazi wazi kama vile; chuki, kulaumu, ugomvi, vurugu, malalamiko, manung’uniko, machafuko, kulipa kisasi au aina yoyote ya uharibifu kutokea kwako au ndani mwako. Hivyo mwanamke shujaa huwa ni heri kila anapokuwa kwani hutunza amani ya eneo alipo.

3.  UPENDO WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa akiishi maisha ya upendo wa halisi na sio wa kinafki kwa jamii inayomzunguka. Tabia ya upendo wa halisi ina thamani kubwa sana kuliko mali nyingi, pesa, elimu ya juu n.k. wewe unaweza kabisa kuwa na elimu ya juu sana na pesa nyingi sana lakini pasipo upendo wa halisi ni sawa na kusema kopo zuri kwa nje na ndani hamna kitu. Nguzo kuu ya maisha ya mwanamke shujaa ni Upendo wa dhati na uhalisia.

4. UTII KWA KWA JAMII:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya utii katika jamii inayokuzunguka  ili kuweza kuyafanyia kazi yale yote uliyojifunza na pia kuyatenda kwa ufasaha pasipo kupita kona yoyote. Utii  kwa jamii ni ufunguo mmoja wapo utakaokusaidia kufanikisha mambo yako na malengo yako kama mwanamke shujaa.

5.  UAMINIFU KATIKA JAMII:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha ya uaminifu wa kweli na uhalisia katika jamii inayomzunguka. Uaminifu wa kweli huonekana nyakati zote na siyo tu wakati mtu anapokuwa mbele za watu wanaomjua bali hata wale wasiomjua na hata anapokuwa mahali peke yake aweze kutunza uaminifu wake kwa faida ya jamii nzima. Mwanamke shujaa hujitahidi sana kutunza uaminifu wake katika sekta zote.

6.  UNYENYEKEVU WA KWELI:
Kila mwanachama anatarijiwa kuishi maisha halisi kabisa ya unyenyekevu kwa jamii inayomzunguka, unyenyekevu ni kinyume
kabisa na kiburi, majivuno, kujigamba, kujikweza, kujiinua, kujiona,
na hata kjitanguliza mbele kwa kila jambo. Mwanamke shujaa huwa ni mnyenyekevu wakati wote na hana makuu daima.

7.  UWAJIBIKAJI WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya uwajibikaji akiangalia majukumu yake yote yanayomkabili na kuhakikisha anafanya kwa moyo bila kuwa na tabia ya kusaidiwa majukumu yake. Mwanamke shujaa ni mfano wa kuigwa kutokana na uwajibikaji wake.

8.  USHIRIKIANO WA DHATI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha halisi ya ushirikiano katika jamii inayomzunguka. Sisi wanawake mashujaa yatupasa kujua dhahiri kuwa kazi ya kubadili tabia na kufanya wengine wabadilike kwa lengo la kupata familia bora ni lazima kuwa na ushirikiano wa kweli ambao utajenga tabia ya kuaminiana na kunai mamoja katika harakati hizi za kuandaa/ kujenga familia bora.

9.   UTARATIBU WA KAZI/MPANGILIO:
Kila mwanachama anatarajiwa kuwa na maisha ya uhalisia katika utaratibu wa maisha yake, pamoja na mpangilio mzuri wa mambo yanayomzunguka hii itakusaidia kuwa na muda mzuri wa kufanya shughuli zako na pia kutekeleza majukumu yako ya kila siku kama mwanamke shujaa. Hakuna njia yoyote ya kukuwezesha kukua na kuendelea katika maisha yako bila kuwa na utaratibu na mpangilio wa mambo yako.
10.  KUFANYA TATHIMINI:
Kila mwanachama anatarajiwa kuishi maisha ya halisi ya kuweza kufanya tathimini ya yale yote anayoyafanya katika maisha yake ya kila siku, pengine ni mfanyabiashara, mfanyakazi, mkulima n.k kama mwanamke shujaa yakupasa kutathimini shughuli zako kama zina leta faida/hasara kwa familia na jamii yako inayokuzunguka. Ukiona faida ni kubwa unaendelea na hiyo shughuli lakini kama hasara ni kubwa unajiweka katika nafasi ya kubadilisha aina ya shughuli mara moja bila kupoteza wakati.





Imeandaliwa na:
Diana Didas Shirima
Founder - Wanawake Mashujaa Tanzania

No comments:

Post a Comment