Thursday, May 31, 2012

USIMUADHIBU MTOTO KWA KUJIKOJOLEA KITANDANI, MSAIDIE KWA KUJUA NINI CHANZO CHA KUMFANYA AJIKOJOLEE NA SI KUMCHAPA!


Ukojozi kitandani unaweza kusababisha matatizo ya kitabia kwa sababu mtoto anaweza kuhisi ana makosa na kujisikia aibu. Ni kweli kwamba mwanao anatakiwa kuwajibika kwa kitendo hicho cha kukojoa kitandani (hii ina maana mwanao anatakiwa kufanya usafi). Lakini usimfanye mwanao ahisi kwamba yeye ndio mwenye makosa.Ni muhimu kwa mwanao kujua kwamba ukojozi kitandani siyo kosa lake. Kitendo cha kumuadhibu mwanao kwa kosa la kukojoa kitandani haitasaidia kutatua tatizo.
Itamsaidia mwanao kujua kwamba hakuna anayejua sababu kubwa inayopelekea ukojozi kitandani.Muelimishe kwamba mambo hayo hutokea katika familia (Kwa mfano, kama mwanao akikojoa kitandani, unatakiwa kujadiliana naye na kumhaidi kumsaidia kupambana na hali hiyo).
Msisitizie mwanao kwamba anatakiwa aende msalani wakati wa usiku. Muwekee taa kuelekea msalani  ili imuwie rahisi kuona njia ya kuelekea msalani. Unaweza pia kumfunika na blanketi pamoja na tandiko lingine la plastiki ili iwe rahisi zaidi wakati wa kufanya usafi.Endapo mwanao atajaribu kukusaidia, msifie kwa kujaribu na kwa kusaidia kufanya usafi.

UKOJOZI KITANDANI KWA WATOTO
 (Bed-Wetting) -Enuresis

Nini maana ya Enuresisi?
Enuresisi ni neno la kitaalamu linalomaanisha hali ya kutoa mkojo bila ridhaa ya muhusika(involuntary),aina mojawapo tuliyoizoea ni ukojozi kitandani wakati mtu akiwa amelala hasa wakati wa usiku.

Ukojozi kitandani huwapata zaidi watoto na mara nyingi ni hali ya kawaida tu katika ukuaji wao. Ukojozi kitandani hutokea zaidi kwa watoto wa kiume kuliko wa kike.

Vitu gani husababisha ukojozi kitandani?
Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha ukojozi kitandani. Baadhi ya njia hizo ni hizi zifuatazo:
  • Kurithi (Katika familia)
  • Kushindwa kuamka kutoka usingizini
  • Msongo wa mawazo
  • Ukuaji wa taratibu wa mishipa za fahamu kutofanya kazi inavyotakiwa 
  • ( hali ambayo humpunguzia mtoto uwezo wa kuzuia kibofu kutoa mkojo)
  • Matatizo ya homoni (kuzalishwa katika kiwango kidogo kwa homoni zinazopunguza kuzalishwa kwa mkojo wakati wa usiku)
  • Maambukizi katika njia ya mkojo
  • Matatizo katika mrija wa mkojo kwa wavulana au kwenye njia ya mkojo kwa wavulana na wasichana.
  • Matatizo kwenye uti wa mgongo
  • Kibofu cha mkojo kuwa kidogo
Ukojozi kitandani sio tatizo la akili au tabia. Tatizo hili halitokei eti kwa sababu mtoto ni mvivu kiasi kwamba hawezi kuamka kitandani na kwenda msalani.

Je ni kipindi gani watoto wengi huweza kudhibiti  hali ya mahitaji ya kukojoa?
Watoto huweza kudhibiti kibofu cha mkojo katika umri tofauti. Wakifikia  umri wa miaka 6, watoto wengi huacha kukojoa kitandani. Ukojozi wa kitandani hadi katika umri wa miaka 6 siyo kitendo cha ajabu, ingawa inaweza kuwanyima amani  wazazi na walezi wengi.Kama mtoto yuko chini ya umri wa miaka 6, tiba kwa tatizo la ukojozi kitandani kwa kawaida siyo mara nyingi watoto wengi huacha kukojoa bila aina yoyote ya matibabu.

Daktari anaweza kusaidia lolote?
Ingawa watoto wengi wanaokojoa kitandani hawana tatizo lolote la kiafya, daktari  anaweza kusaidia kugundua kama tatizo la mtoto wako kukojoa kitandani linasababishwa na matatizo mbalimbali ya kiafya. Kwanza daktari atakuuliza iwapo mwanao hukojoa mchana na usiku. Halafu daktari atampima na anaweza kuchukua vipimo vya mkojo kuangalia kama kuna maambukizi au kisukari au matatizo mengine.
Daktari anaweza kutaka kujua mwenendo wa kimaisha wa mwanao anapokuwa nyumbani na hata shuleni.Ingawa unaweza kuogopa mtoto wako anapokojoa kitandani, tafiti zimeonyesha kuwa sio rahisi kwa watoto wanaokojoa kitandani kuwa na matatizo ya hisia tofauti na watoto wengine wasio kojoa kitandani.Daktari pia atakuuliza jinsi mnavyoishi katika familia kwa sababu m matibabu  yanaweza kuhusisha mabadiliko kadhaa ya kimaisha hapo nyumbani.

Je kuna matibabu yoyote  kwa tatizo la ukojozi kitandani?
Watoto wengi huacha kukojoa kitandani bila kupata matibabu yoyote.Ingawa wakati mwingine wewe na daktari wako anayemuona mtoto wako mnaweza kuamua kwamba mtoto anahitaji tiba fulani.Kuna aina 2 za tiba: kumbadili mtoto kitabia, na kumpatia dawa. Kumbadili mwanao kitabia husaidia kumfanya mwanao aache tabia ya kukojoa kitandani.Baadhi ya njia za kumbadili mwanao kitabia ni hizi zifuatazo:
  • Mzuie mwanao asinywe vinywaji/maji kwa wingi kabla ya kulala
  • Hakikisha mwanao anenda msalani kila mara kabla ya muda wa kulala na pia mara tu anapo anza kusinzia.
  • Tumia kengele itakayolia pindi kitanda kinapolowa ,hii humfundisha mtoto kufahamu pindi kibofu kinapojaa wakati wa usiku
  • Mpe zawadi mtoto anapoamka bila kukojoa kitandani
  • Mwambie mtoto wako kubadili matandiko mwenyewe kila anapokojoa kitandani
  • Mpe mwanao mazoezi ya kibofu: muelekeze mwanao akae muda mrefu bila kukojoa kipidi cha mchana, ili kibofu kiwe na uwezo wa kutunza mkojo mwingi zaidi      
Ni dawa gani zinazotumika kutibu ukojozi kitandani?
Daktari wako anaweza kumpa mwanao dawa kama ana umri wa miaka  zaidi ya saba(7) iwapo njia za kumbadilisha kitabia zilizotajwa hapo hazijasaidia. Hata hivyo dawa hazitibu ukojozi kitandani, Aina mojawapo ya dawa husaidia kibofu kutunza mkojo zaidi, na dawa nyingine husaidia figo kutengeneza kiwango kidogo cha mkojo. Dawa hizi zinaweza kuwa na madhara kiafya kwa mfano, mdomo kukauka na mashavu kuwa na rangi nyekundu.

No comments:

Post a Comment