KUMJENGEA MTOTO HESHIMA BINAFSI "Self-esteem"
Heshima binafsi (Self-esteem) ni
ngao ya mwanao dhidi ya changamoto nyingi za dunia hii. Watoto wengi
wanaojivunia uwepo wao ndani ya familia au mahali fulani mara nyingi wamekuwa
na uwezo wa kutatua migogoro na kuzuia misukumo hasi kirahisi.
Watoto wa aina hii kila mara huwa
wanatabasamu na kufarahia maisha. Watoto hawa huwa wapo wazi hawaoni aibu na
wanaari ya mafanikio muda wote.
Kwa upande mwingine, watoto wasio au
wenye heshima binafsi dhaifu, wanaweza kuchukulia changamoto wanazopambana nazo
kama chanzo cha wasiwasi na mara nyingi hukata tamaa. Wale wenye fikra mbovu
kuhusu wao wenyewe huwa wanapata wakati mgumu sana kutatua matatizo mbalimbali.
Ukimpa suala la kufikiria sana akupe
jibu mfano “mimi mbaya” au “siwezi kufanya lolote vyema” atakaa kimya,
ataondoka au atafadhaika tu kimya kimya. Akikutana na changamoto yoyote jibu
lake la haraka ni “siwezi mimi”.
Jinsi ya kumwezesha mwanao
kujijengea heshima-binafsi.
Heshima binafsi na
kujiamiani ni nini?
Heshima binafsi ni mkusanyiko wa
imani au hisia tulizo nazo kuhusu sisi wenyewe, yaani tunavyojitambua.
“Tunavyojielezea wenyewe mbele ya
wenzetu tunashawishi vichocheo binafsi ndani yetu, fikira na tabia na tunagusa
jinsi tunavyoweza kurekebisha au kuikabili mihemko yetu.
Utaratibu wa kumjengea mtoto heshima
binasfi na kujitambua huanzia utotoni. Mfano, mtoto anayefikia lengo fulani
kama kuwa wa kwanza darasani anajijengea ujasiri unaoimarisha heshima binafsi.
Mtoto anapobadili maamuzi na kutafuta njia nyingine ya kutekeleza nia yake
baada ya kujaribu na kushindwa kufanya kitu fulani mara kadhaa kunamjengea
fikira za “ninaweza”.
Dhana ya mafanikio ya mtu kulingana
na msimamo wake huanzia utotoni. Jinsi mtoto anavyojaribu na kushindwa,
anajaribu tena na kushindwa tena na hatimaye kufanikiwa anajijengea uwezo
binafsi wa kujiamini. Wakati huo huo, mtoto huyu anajijengea ufahamu binafsi na
ujasiri wa jinsi ya kujichanganya na watu wengine.
Ndio maana kuhusishwa kwa
mzazi katika makuzi na malezi ya mtoto ndio njia pakee na sashihi ya kuwasadia
watoto kujijengea ufahamu binafsi. Heshima binafsi pia inamaanisha hisia za
kuweza, kulikochanganyika na hisia za kupendwa. Mtoto anayefurahia mafanikio
fulani lakini wazazi wake hawaonyeshi kufurahia mafanikio hayo, mtoto huyo
atapungukiwa na heshima binafisi na kujiamini.
Vilevile, mtoto anayehisi kupendwa
lakini anaona aibu kuhusu uwezo wake pia anaweza kupungukiwa heshima binafsi.
Heshima binafsi huja pale tu kunapokuwa na usawa kwenye haya mawili, yaani
kutoona aibu kwa kujiamini na kuhisi anapendwa.
Dalili za heshima bora na
heshima dhaifu kwa mtoto
Heshima binafsi inabadilika
kulingana na mtoto anavyokua. Hubadilika na kuboreshwa mara kwa mara kwa sababu
huchangiwa na uzoefu wa mtoto na ufahamu mpya anaoupata. Hivyo inamsaidia
kuzitambua dalili za heshima bora na heshima dhaifu.
Watoto wanaopungukiwa heshima binafsi
hawapendi kujaribu mambo mapya na mara nyingi hujishusha kuhusu uwezo wao
wenyewe. “mimi mbumbumbu”, “Siwezi kujifunza namna ya kufanya hili” au “hakuna
anayenijali”. Hawawezi kuhimili vipingamizi, hushindwa mapema na mara nyingi
hutegea mwingine afanye.
Watoto wenye heshima binafsi na
wanaojiamini hupenda kujichanganya na wengine. Hufurahia jamii inayowazunguka
na shughuli zinazoendelea ndani ya jamii, mara nyingi huwa ni wadadisi wa
mambo. Inapotokea changamoto, hujitahidi kupata ufumbuzi na huonyesha
kutoridhika na mafanikio wanayoyapata bila ya kudharau wengine. Mfano, badala
ya kusema ‘mimi zuzu’ mtoto mwenye heshima binafsi ya kujiamini atasema ‘hili
silielewi’ wanajua mapungufu na uwezo wao na wanakubali hali walio nayo.
Wazazi wanawezaje kusaidia
Je, mzazi anawezaje kumsaidia mwanae
kujijengea heshima binafsi na kujiamini? Vigezo vifuatavyo vinaweza kusaidia:-
1. Chunga unachoongea
Watoto wako makini sana na maneno
wanayoongea wazazi wao. Kumbuka kusifia mwanao si kwa kazi nzuri tu aliyoifanya
lakini pia kwa jitihada anazoonyesha katika kufanikisha jukumu fulani. Lakini
inampasa mzazi kuwa mkweli. Mfano, kama mwanao amefeli darasani labda ameshika
namba 28 kati ya watoto 30, unaweza kumsifia tu kama mwanzoni alikuwa wa 30.
Lakini kuwa mkweli kwamba matokeo yako bado ni mabaya sana.
2. Kuwa mfano bora
Kama wewe mzazi unatabia za ukali,
matusi, umekata tamaa na huonyeshi matumaini (kukosa rajua), au si mkweli
kuhusu uwezo wako kama mzazi, mwanao anaweza kuakisi tabia zako.
Onyesha heshima na nidhamu kama
mzazi na mtoto atajifunza kutoka kwako.
Watoto huwa wanaamini baadhi ya
mambo ambayo si mazuri katika makuzi yao. Ni jukumu la mzazi kuzitambua imani
potofu alizonazo mwanae na kutafuta jinsi ya kumwanisha ukweli. Mtoto anaweza
kuamini kuwa mtoto ananunuliwa na hazaliwi, jaribu kutafuta mbinu za
kumwaminisha ukweli kadiri anavyokua.
Mfano, mtoto anayefanya vizuri
darasani lakini anashindwa kwenye somo la Hisabati, anaweza kusema ‘siwezi
kufanya hesabu’ mimi sio mwanafunzi mzuri. Imani ya mtoto kujumuisha kushindwa
hesabu darasani na kutokuwa mwanafunzi mzuri darasani ni imani potofu.
Ukimwacha mtoto akue na imani hiyo inaweza kupelekea kushindwa baadae hata
kwenye maisha yake.
Mpe moyo mwanao, mwambie ‘wewe ni
mwanafunzi bora’ unafanya vizuri shuleni, Hesabu ni somo moja tu, jifunze tu
sana Hesabu utailewa.
3. Onyesha wazi unampenda
mwanao
Upendo unaouonyesha kwa mwanao
utasaidia kumjenga kwenye kujiamini na kuimarisha heshima binafsi. Wakumbatie
wanao na waonyeshe kuwa unawafurahia.
Tafuta urafiki wa karibu na mwanao.
Kuwa karibu nae kwa kadiri iwezekanavyo hata kama unabanwa na kazi lakini weka
mipaka pia kwenye mapenzi unayoyaonyesha kwa wanao. Watoto ni wepesi sana
kutambua kama mzazi anampenda kweli au hampendi.
Ni vyema umwambie alivyo fahari yako.
Andika ujumbe kuelezea unavyomchukulia na uweke mahali atakapouona ghafla akiwa
mwenyewe kama vile kwenye mfuko/begi lake la shule, kitandani kwake na
kwingineko. Atafurahi kila anapoona ujumbe huo.
4. Jenga mazingira safi ya
malezi
Mtoto asiyejisikia salama au yule
anayejiona kuwa ananyanyaswa nyumbani anaweza kujihisi yu duni. Mtoto
anayelelewa na wazazi wanaogombana mara kwa mara, hukata tamaa na mwenendo wa
maisha.
Watoto wa aina hii hupoteza hamu ya
kuwa nyumbani kiasi kwamba hujiona wenye balaa kuzaliwa na nyie wazazi. Anaweza
kujenga chuki zisizotawalika na akawa mgomvi na mbishi dalili za
kujifikiria-dhaifu. Jaribu kuchunguza ikiwa mwanao ameudhiwa huko alikokuwa,
kama vile shuleni ama na marafiki zake, mwulize maswali yatakayokupa picha
ikiwa yeye ndiye tatizo yeye ndio chanzo cha ugonvi. Halafu mpe ushauri nasaha
kwa zingatio hilo.
5. Msaidie mwanao ajifunze
kujaribu
Ni jukumu la mzazi kujishughulisha
sana katika kumsaidia mtoto wake awe na tabia ya kujaribu mambo. Shughuli
zinazosisitiza ushirikiano wake na wenzake ni nzuri zaidi ya zile zilizokaa
kimashindano zaidi. Kwa hiyo kama una watoto zaidi ya mmoja, ni vyema
ukawapangia majukumu yanayofanya washirikiane. Kwa mfano, unaweza kumshauri
aliye mkubwa asaidie kumfundisha mdogo wake kusoma ama kufanya hesabu. Ukiwapa
kazi zenye mwelekeo wa kimashindano unaharibu. Yule ashindaye atajenga kiburi,
majigambo na dharau na yule ashindwaye atajiona hawezi hasa kama zoezi hili
limejirudia mara kadhaa.
6. Tafuta msaada wa
wataalam
Ukiona mwanao anajengeka na kukua
kwa kutojiamini, amua kutafuta ushauri wa wataalam. Wapo washauri nasaha wenye
uwezo wa kumtambua mwanao na kukushauri ni kwanini anashindwa kujiamini au
kujijengea heshima binafsi kwenye jamii inayomzunguka.
Hivyo, sisi wazazi tunanafasi kubwa na
muhimu sana ya kuwafanya watoto wetu kujenga uwezo wa kujiamini na kuwa na
heshima binafsi kuhusu maisha yao mwenyewe. Na wazazi tusipokuwa makini kwa
matendo yetu jinsi tunavyowalea watoto wetu, tunawajengea udhaifu wa kujiamini
hata watakapokuwa wakubwa mbele za watu.
SAIKOLOJIA NA TABIA
Maisha ya kifamilia yanapitia mambo
mengi. Ni jukumu letu sisi wazazi kumtayarisha mtoto ili aweze
kukabiliana nayo. Mambo hayo yanaweza kuwa wazazi kuachana, kifo cha mzazi
mmojawapo au wote, kuzaliwa kwa mtoto mwingine, tabia ya nyumbani kukiwa na
wageni na kadhalika. Mtoto anastahili matayarisho ya kisaikolojia kuhusu mambo
hayo. Pia jua tabia mbalimbali za mtoto kwa jinsi anavyokua hadi kufikia ujana.
Kumfunza mwanao nidhamu
Utafanyaje kumuepusha mwanao
asiangalie video kwa muda mrefu kama ameshazoea? Je, mwanao akiwa shuleni kama
mwanafunzi mwenzake akianzisha fujo mfano amempiga ngumi, afanyeje? na ufanyeje
ili mwanao aheshimu mamlaka yako kama mzazi? Haya ni baadhi tu ya masuala
ya msingi ambayo wazazi wengi tumeshindwa kuelewa madhara yake katika kujenge
nidhamu ya mtoto.
Ni vyema mzazi uwe na msimamo ambao
uko wazi kwa mwanao. Ukiongelea masuala ya mzaha iwe ni mzaha kweli,
linapokuja suala la nidhamu uonyeshe unamaanisha nidhamu kweli. Kama maamuzi
unayofanya yanakinzana kila mara hata mwanao ni vigumu kuyafuata.
Katika sehemu hii tunaeleza jinsi
unavyoweza kuweka nidhamu ya watoto wako ndani ya familia. Nidhamu unayotakiwa
kuijenga hutofautiana kati ya mtoto na mtoto kulingana na umri.
Mwaka 0 hadi miaka 2
Watoto wa umri huu mara nyingi
hutaka kushika kila kitu, kumbuka ni umri huu ambapo mtoto anatambaa, anaanza
kutembea, anaanza kuongea na anaanza kula vyakula mbalimbali ni vyema kuweke
mbali vitu vinavyowapeleka kwenye majaribu ya kutaka kufanya jambo fulani mfano
kuwasha TV, redio, kugusa vitu vya thamani, kula vitu anavyookota, dawa nk.
Vitu hivi ni muhimu viwekwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufikia.
Mzoeshe mwanao anayetambaa
kumkataza, mwambie “ACHA” au “HAPANA” anapotaka kushika vitu hatari au vitu ambavyo
unawasiwasi anaweza kuviharibu au vinaweza kumletea madhara na mtoe eneo hilo.
Tusiadhibu watoto wetu wa umri
wowote kwa kuwapiga au kuwachapa viboko, mtoto hawezi kuhusisha viboko na kosa
alilotenda zaidi ya kuhisi tu maumivu ya fimbo.
Watoto wetu wanajifunza kutokana na
yale tunayoyafanya kama wazazi, ni jukumu la mzazi kujaribu kuwa mfano wa
kuigwa. Watoto ambao wamezoea kuona mama na baba daima ndani ni ugomvi,
kupigana na matusi, watoto hao hawana amani na mara nyingi huishia kuiga tabia
mbaya kutoka kwa wazazi hawa.
Miaka 3 hadi 5
Mtoto wa umri huu anaanza kujifunza
na kuelewa mema na mabaya kutokana na matendo yake. Kuanzia umri huu anza
kumfundisha mtoto sheria na taratibu za familia yako. Mfano kumsalimia baba na
mama kila anapoamka asubuhi au kusema asante baada ya chakula au anapowewa
kitu, kusalimia watu wanaomzidi umri nk.
Unapowapa watoto wa umri huu onyo au
karipio waeleze kwanini kosa alilofanya ni kosa au kwanini alivyofanya si
sahihi. Mfano mtoto amechora ukuta kwa rangi, mwambie rangi za kuchorea ni kwa
ajili ya karatasi si kwa ajili ya ukuta na mwambie ukichora ukuta unaharibu
mwonekano mzuri wa ukuta, hivyo asirudie.
Wakati unawajengea watoto ufahamu wa
kipi ni kibaya ambacho wakifanya wataadhibiwa, ni vyema pia uwajengee nidhamu ya
kuelewa kuwa ni mambo gani ambayo wakiyafanya vizuri watapata zawadi au wewe
kama mzazi unayafurahia. Mfano, wazoeshe watoto umuhimu wa kufanya vizuri
darasani. Waambie umuhimu wa kusoma, wajengee hamu ya kutaka kufika Chuo Kikuu
nk na uwaeleze faida zake.
Watoto wa umri huu wanapokosa
unaweza kuwapa adhabu kama vile kumtenganisha na vitu fulani fulani ili
kumjengea mtoto wa umri huu tabia nzuri. Mtenganisshe kwa muda ni vitu
kama vile, kumzuia mtoto kungalia TV, kusikiliza redio, kucheza na wenzake kwa muda
fulani nk.
tumekupata mama familia,asante kwa mafundisho haya,
ReplyDeleteAhsante Neema karibu sana ujiskie upo huru na blog hii kuuliza au kutoa mada yoyote inayohusu familia na malezi ya watoto ili tusaidiane katika kulea watoto wetu vizuri.
Delete