Thursday, May 31, 2012

KUJIFUNGUA NA TARATIBU ZAKE, JE WAZIJUWA?


Baada ya kufikisha miezi tisa au kitaalamu tunahesabu majuma 40, mama mjamzito anajifungua au anazaa mtoto.

Kabla ya kuzaa, mama anapata uchungu kutokana na kutanuka kwa nyonga, kufunguka mlango wa uzazi na msukumo wa mfuko wa uzazi “uterine contractions”. Baada ya hapo maji maji na damu nyepesi vitatoka “rupture of membrane”.  Chupa ikipasuka ndipo mtoto anapotoka. Mtoto anaweza kutoka kwa kutanguliza kichwa “cephalic presentation” au akatanguliza matako “breech presentation” au mtoto anaweza kutanguliza mikono au miguu au uso,lakini yote haya yatarekebishwa wakati wa kujifungua.

Wakati wa kujifungua uchungu unaweza kuwa mkali au wa wastani au mama anaweza kupata uchungu halafu ukapotea hivyo jitihada zingine zitafanyika. Pia mama anaweza kupata matatizo wakati wa kuzaa ambapo njia itakuwa haifunguki au nyonga kutoruhusu mtoto kupita, pia hapa jitihada zitafanyika.

Mama anatakiwa ahudhurie kliniki sehemu ambayo kuna wataalamu mfano katika vituo vya Afya na Hospitali kubwa. Akithibitika kuwa ana matatizo ya kiafya na anatakiwa ahudhurie kliniki katika Hospitali kubwa, basi ni vema kufanya hivyo.

Kuna baadhi ya sehemu kunakuwa na uhaba wa vifaa vya kujifungulia hivyo ni vema kabla mama hajaenda kujifungua akapata maelekezo kliniki ya vifaa vinavyohitajika. Kujifungua kupo kwa aina mbili kuu ambapo kuna kujifungua kwa njia ya kawaida, au endapo kuna tatizo basi hujifungua kwa njia ya operesheni au siza.

Zipo njia zingine za kusaidia kujifungua kawaida kama vile za kumvuta mtoto kwa kifaa maalum “vacuum” au mama kuongezwa njia.

 Njia hizi zina faida na hasara. Faida ni mtoto kuwahi kuzaliwa na kumpunguzia mama uchungu.
Hasara yake inaweza kuwa mtoto anapovutwa anaweza kuumizwa kichwa hivyo kupata matatizo ya ubongo na akili kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment