Monday, May 28, 2012

WANAWAKE WAJAWAZITO MPOO?

AFYA NA VYAKULA KWA MAMA MJAMZITO
Mara tu mama anapokuwa mjamzito ni vema awahi kuhudhuria  kliniki. Mimba huchukua majuma 40 au miezi 9.Kipindi cha ujauzito kimegawanyika katika miezi mitatu au “tri-semister”. Katika vipindi  hivi kuna mabadiliko mbalimbali yanayoweza kuathiri afya ya mama.

Mama mjamzito anatakiwa awe na afya njema kabisa katika kipindi cha ujauzito.Tukizungumzia afya njema tunamaanisha afya ya akili na mwili. Mama asiwe na matatizo yoyote yatakayomuathiri kisaikolojia pia mwili wake uwe imara nawenye nguvu.

Ili kuwa na afya njema kimwili mama anatakiwa ale chakula bora “Balanced Diet”. Chakula bora ni chakula ambacho kina  aina  kuu  tatu za vyakula; kwanza  ni chakula cha kujenga mwili ambapo mwili wa mama na mtoto aliye tumboni unatakiwa ujengwe na uendelee kujengwa.Vyakula vya kujenga mwili ni vile vya protini ambavyo ni vya aina zote,  samaki aina  zote ili mradi nyama na samaki hizo hazimdhuru mama na wala havina miiko kwake.

Vyakula vingine vya kujenga mwili ni mayai, maharage, kunde, karanga, soya, mbaazi na jamii yoyote ya kunde au maharage.

Aina ya pili ya  chakula bora ni kinacholinda mwili. Mwili wa mama mjamzito na mtoto aliye tumboni ni vema ulindwe dhidi ya maradhi mbalimbali ya kuambukiza. Maradhi ya kuambukiza ni kama vile yale ya njia ya hewa na mkojo,pia hata udhaifu wa mwili.
Mafua, kikohozi,UTI, maumivu ya tumbo,misuli, mifupa yote yanaweza kutibiwa au kuzuiliwa kwa kula vyakula vya kulinda mwili. Vyakula hivi pia husaidia kuongeza damu na kuzuia upungufu wa damu.Vyakula hivi ni vitamini na madini.

Vitamini zinazotumika kuimarisha mwili ni vitamin A,B,C,D,E,na K , kila vitamini ina kazi yake lakini kazi kuu ya vitamini ni kulinda mwili.
Madini yanayotumika mwilini ni madini ya chokaa au calcium, zink, madini ya chuma ,potassium,manganese,chloride ,sodium, magnesium. Madini  ndiyo yanayosaidia kuimarisha mwili na kuongeza damu.

Vitamini na madini  hupatikana katika mboga za majani na matunda. Madini pia hupatikana katika nyama kama maini, figo,mayai, samaki, hasa dagaa ,mafuta ya samaki, vyakula vya kutia nguvu ni aina ya tatu  kuu ya chakula bora. Vyakula  hivi ni vile vya  mwanga mfano ugali, na wali, mihogo, mtama, ulezi,uwele, mahindi, na ndizi.
Ulaji wa vyakula hivi huufanya mwili uwe na nguvu na kumwezesha mama mjamzito kushiriki katika shughuli nyingine za uzalishaji mali.

No comments:

Post a Comment